2015-03-19 12:00:00

Askofu mkuu Lingua kuendeleza diplomasia nchini Cuba


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Giorgio Lingua kuwa Balozi mpya wa vatican nchini Cuba. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Lingua likuwa ni Balozi wa Vatican nchini Iraq na Yordan ambako ameshuhudia mateso na mahangaiko ya Wakristo kutokana na nyanyaso na dhuluma za kidini, lakini wakati wote amejitahidi kuwa ni rejea ya matumaini kwa wale waliokata tamaa. Anaondoka Iraq ambako bado damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika!

 

Askofu mkuu Lingua alianza huduma ya kidiplomasia mjini Vatican kunako mwaka 1992. Tangu wakati huo ametekeleza utume wake sehemu mbali mbali za dunia kama vile: Pwani ya Pembe, Marekani, Serbia na Italia. Amewahi kufanya kazi katika Sekretarieti ya Vatican kwenye idara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican na alijikita zaidi kwa masuala yaliyokuwa yanazihusu nchi za Amerika ya Kusini na Caribbeani.

 

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Lingua anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Askofu mkuu Bruno Musarò aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi wa Vatican nchini Misri. Askofu mkuu Lingua ameteuliwa kwenda Cuba wakati huu wa kipindi cha mageuzi makubwa ya mahusiano na mfungamano wa kimataifa kati ya Cuba na Marekani, ambao wako kwenye mchakato wa kurejesha tena mahusiano ya kidiplomasia baada ya nchi hizi mbili "kutuniana misuri" kwa zaidi ya miaka 50.

 

Anakwenda kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidiplomasia ulionzishwa na Vatican na kwa sasa cheche za uvumilivu na matumaini zinaanza kuonekana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.