2015-07-13 11:02:00

Mabadiliko ni dhana inayowezekana, watu wakipania!


Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Amerika ya Kusini kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 13 Julai 2015 kwa kutembelea Equador, Bolivia na Paraguay imekuwa na mafanikio makubwa. Baba Mtakatifu Francisko ameionesha Familia ya Mungu Amerika ya Kusini kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kufanya mabadiliko, ikiwa kama kweli watu wanapania.

Ni maneno ya Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican ambaye amekuwa bega kwa bega na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume huko Amerika ya Kusini, akijaribu kutoa muhtasari wa mambo makuu yaliyojiri wakati wa hija ya Baba Mtakatifu Francisko huko Amerika ya Kusini. Watu wameomwonesha Baba Mtakarifu ukarimu na upendo wa ajabu kwa kumpatia mapokezi makubwa na bila mzaha, akawaonjesha ule upendo wa kibaba; kwa kuwatia moyo na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi, tayari kujifunga kibwebwe kupambana na baa la umaskini wa hali na kipato; ukosefu wa usawa na tatizo la baadhi ya watu kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko amewaachia wananchi wa Amerika ya Kusini katika ujumla wao, ujumbe wa matumaini yanayojikita katika mabadiliko ya maisha na kwamba, hata Kanisa katika maisha na utume wake, linapaswa kujikita katika mchakato wa mabadiliko, kwa kuonesha upendo na mshikamano; kwa kuwatangazia watu Injili ya  Furaha na Huruma ya Mungu; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, mafao na haki msingi za binadamu.

Sera na mikakati ya maendeleo ya kiuchumi, itoe kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na wala si faida za kiuchumi na kisiasa. Mageuzi haya ya maisha yanapaswa kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume, ametangaza na kushuhudia Injili ya Furaha, kauli mbiu inayoongoza maisha na utume wake. Huu ni ukweli wa Injili unaogusa undani wa maisha ya mwanadamu na kuwachangamotisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufanya maamuzi ya kina kwa ajili ya mafao ya wengi.

Padre Lombardi anakiri kwamba, hija hii ilikuwa ni ndefu na yenye kuchosha, lakini kwa njia ya utashi kamili, nguvu na ujasiri wa Baba Mtakatifu Francisko, yote yamekwenda barabara, matendo makuu ya Mungu. Baba Mtakatifu ameonesha ujasiri wa kukabiliana na changamoto mbali mbali, kwa kuzingatia pia umri wake, kiasi cha kutekeleza ratiba iliyopangwa wakati wa hija yake ya kitume. Kwa hakika, amejitosa kimasomaso kutangaza na kushuhudia Injili na kwamba, neema, baraka na upendo wa Mungu umewezesha kufanikisha yote haya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.