2015-07-15 09:42:00

Washirikisheni watu Injili ya Furaha kama sehemu ya Uinjnilishaji mpya!


Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, hivi karibuni limeadhimisha kongamano la kitaifa kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya, tukio ambalo limehudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu nchini Uingereza. Ni waamini ambao walikuwa na kiu ya kutaka kufahamu mbinu za Uinjilishaji mpya zinazojikita katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo yenye mvuto na mashiko, ili hatimaye, kuweza kuyatakatifuza malimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Baraza la Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles anakaza kusema, hii ni fursa muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, si tu katika kutafakari na kufanya upembuzi wa kina kuhusiana na mikakati ya shughuli za kichungaji, bali ni fursa ya kuwasha moto wa upendo, furaha, imani na matumaini miongoni mwa waamini, kwa kukutana na Yesu Kristo mkombozi wa dunia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza linataka Parokia ziwe ni vitalu vya Uinjilishaji mpya, tayari kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo. Hili ni kongamano ambalo limehudhuriwa na mihimili ya Uinjilishaji nchini Uingereza na Walles, kama sehemu ya mchakato wa kumwilisha changamoto zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, Injili ya Furaha, “Evangelii gaudium”  unaoonesha dira na vipaumbele vya Kanisa Katoliki katika mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Kardinali Vincent Gerald Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles anasema kwamba, kongamano hili limekuwa ni fursa kwa Familia ya Mungu nchini Uingereza kuimarisha mahusiano yao na Yesu Kristo, Bwana na Mwalimu, tayari kutoka kimasomaso kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Hii ni changamoto ya kujikita katika sala, tafakari na Neno la Mungu na matendo ya huruma; mambo msingi ambayo waamini wanaweza kuwashirikisha jirani zao kama sehemu ya Uinjilishaji mpya.

Waamini wanaalikwa kuwa ni mashuhuda wa Injili ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo, lengo ni kuwawezesha waamini ambao wamepoteza dira na mwelekeo wa maisha ya Kikristo kuona tena mwanga na cheche za Habari Njema ya Wokovu. Hawa ni walengwa wa kwanza katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Pili, ni kuamsha udadisi miongoni mwa watu na hapo kuweza kumwachia Roho Mtakatifu kutenda kazi yake, hata kama waamini watakutana na kinzani pamoja na changamoto za maisha.

Kardinali Nichols anasema, tatu ni kumsaidia mwanadamu anayeelemewa na vurugu, kinzani,  mahitaji na hasira, ili kuunganisha kilio hiki na sala za waamini, kutoka sehemu mbali mbali za dunia; ili kushiriki kikamilifu katika utume wa Uinjilishaji unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Familia ya Mungu nchini Uingereza inaendelea kugundua kwamba, inahitaji kuzima kiu ya uwepo wa Mungu kati yao, kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya kimaadili, kijamii, kiutu na kitamaduni.

Familia ya Mungu nchini Uingereza anasema Kardinali Nichols inajisikia kana kwamba, imeacha njia sahihi katika maisha na kwas asa inataka kuanza tena mchakato wa kuitafuta na kuiambata katika maisha. Hii ndiyo kazi kubwa inayopaswa kufanywa na mchakato wa Uinjilishaji mpya. Watu watambue kwamba, imani kwa Mwenyezi Mungu ni rasilimali inayopaswa kukuzwa na kuendelezwa, changamoto kwa waamini kujifunza mbinu za kuwashirikisha wengine ile furaha ya imani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.