2015-07-20 13:18:00

Kuna watu wanaoendelea kutanua maisha kwa fedha inayonuka damu ya watu


Baraza la Maaskofu Katoliki Japan kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kumalizika kwa Vita kuu ya Pili ya Dunia iliyosababisha majanga makubwa kwa wananchi wengi duniani, lakini kwa namna ya pekee kwa wananchi wa Japan, pale walipofumba na kufumbua wakakuta miji ya Hiroshima na Nagasaki, imepigwa mabomu ya atomiki na kugeuka kuwa majivu ya hatari katika maisha ya mwanadamu.

Maaskofu wanasema, kuna maelfu ya watu ambao wameathirika kutokana na mashambulizi ya mabomu ya Nyuklia nchini Japan, lakini cha kushangaza hata leo hii bado kuna watu wanaotaka kusababisha vita pamoja na kutaka kutumia silaha za maangamizi.

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, katika ulimwengu wa utandawazi kuna watu ambao hawaguswi na shida wala mahangaiko ya watu wengine, ni watu waliojikita katika biashara haramu ya silaha inayoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao sehemu mbali mbali za dunia. Idadi ya maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii inazidi kuongezeka maradufu, wakati huo huo kuna kikundi kidogo cha watu wanaoendelea kutanua kwa fedha ya damu ya watu wasiokuwa na hatia!

Ikiwa kama kweli, Jumuiya ya Kimataifa inataka kupata haki na amani ya kudumu, kuna haja ya kubadili mwenendo na mwelekeo wa maisha. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan kunako mwaka  1995 na mwaka 2005 liliandika barua ya kichungaji kuitaka Familia ya Mungu nchini humo, kuhakikisha kwamba, inajikita katika ujenzi wa tunu msingi za haki na amani.

Vita kuu ya Pili ya Dunia imeacha kurasa chungu katika maisha ya watu wengi duniani, lakini Japan ilikiona cha mtema kuni. Hiroshima na Nagasaki ni makovu ya mabomu ya atomiki ambayo hadi leo hii yanaendelea kusababisha mateso makali kwa watu wasiokuwa na hatia. Athari hizi, zimejenga ndani ya watu wenye mapenzi mema hamu ya kutaka kutafuta, kujenga na kudumisha misingi ya amani, kiasi cha wananchi wa Japan kuandika hamu hii katika Katiba ya Nchi ambayo ni sheria mama, iliyopitishwa kunako mwaka 1946.

Kwa njia ya mwelekeo huu, Japan ikaanza mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na urafiki na nchi mbali mbali Barani Asia. Kanisa wakati wote huo lilikuwa linapinga uwepo endelevu wa vita baridi na matokeo yake ni kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, nchini Ujerumani, kielelezo cha chuki na utengano kati ya Watu wa Mataifa. Kanisa linaendelea kupinga vita kama suluhu ya migogoro na kinzani kati ya Watu wa Mataifa.

Ndiyo maana, Mtakatifu Yohane XXIII ataendelea kukumbukwa kwa Waraka wake wa kichungaji, Amani Duniani, Pacem in Terris na changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II dhidi ya vita na badala yake, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika Injili ya Amani na Maridhiano kati ya watu. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linabainisha kwamba, Kanisa lina wajibu, utume na dhamana ya kusaidia mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha amani, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Maaskofu wanasema wanaendelea kusali na kuombea amani si kama tatizo la kisiasa bali changamoto muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Vita ni udhalimu dhidi ya ubinadamu. Maaskofu Katoliki Japan wasingependa kuona Serikali yao kwa njia ya kupindisha Katiba, inajiingiza katika vita.Mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia yanatisha na kusikitisha sana sanjari na uchafuzi wa mazingira ambao umeleta athari kubwa sana katika mabadiliko ya tabianchi. Baba Mtakatifu Francisko anasema mambo yote haya ni cheche za vita ya tatu ya dunia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Japani linabainisha kwamba, miaka 70 tangu kusitishwa kwa Vita kuu ya Pili ya Dunia na Miaka 50 tangu kuhitimishwa kwa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, iwe ni fursa ya kuchuchumilia mchakato wa ujenzi wa amani duniani.Waamini wa Kanisa Katoliki Japan ni wachache, lakini wanapenda kuungana na Familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia kutafuta amani na kuendeleza amani, ili kweli amani iweze kustawishwa katika akili na mioyo ya watu, kwani amani ni jina jipya la maendeleo endelevu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.