2015-07-22 08:11:00

Serikali ya Zambia yapongezwa kwa kujikita katika maendeleo ya watu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia linaipongeza Serikali ya Zambia kwa kusimama kidete kushughulikia kero na changamoto za kijamii zinazowatesa wananchi wengi wa Zambia pamoja na kuendeleza mchakato wa maendeleo unaopania kuwaletea wananchi wa Zambia maendeleo endelevu. Haya ni maneno ya shukrani yaliyotolewa na Askofu Alick Banda wa Jimbo Katoliki Ndola, Zambia, alipokuwa anazungumza na Rais wa Zambia Edgar Lungu kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia.

Pale panapojitokeza mambo mazuri, ukweli unapaswa kusemwa ili kuwatia moyo watu wanaojibidisha kukoleza maendeleo ya wananchi wa Zambia, licha ya athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Utu, heshima na maendeleo ya wananchi wa Zambia katika ujumla wao ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu.

Kanisa linatambua na kuthamini mchango unaotolewa na Serikali katika mchakato wa maboresho ya uchumi, miundo mbinu, elimu, afya na maisha ya wananchi wa Zambia. Hii ni changamoto kwa wananchi wa Zambia kuendelea kujenga na kushikamana kama taifa moja. Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia linakaza kusema, kitaendelea kushirikiana na Serikali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Zambia: kiroho na kimwili.

Kanisa linaiomba Serikali ya Zambia kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kulinda na kuendeleza utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote na kwamba, madini na rasilimali ya taifa zitumike kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi badala ya kuwanufaisha watu wachache ndani ya jamii. Maaskofu wanaishauri Serikali ya Zambia kuwekeza katika teknolojia rafiki pamoja na kuanza mchakato wa maboresho ya sekta ya afya, ili kulinda na kudumisha afya za wananchi wa Zambia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.  








All the contents on this site are copyrighted ©.