2015-10-27 09:27:00

Marehemu Kard. Korec alikuwa mchungaji mahiri, mkarimu na mwaminifu kwa Injili


Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam za rambi rambi kwa Askofu mkuu Stanislav Zvolensky kufuatia kifo cha Kardinali Jàn Chryzostom Korec kilichotokea hapo tarehe 24 Oktoba 2015, akiwa na umri wa miaka 91. Marehemu Kardinali Korec atazikwa tarehe 31 Oktoba 2015 Jimboni Nitra, nchini Slovakia. Ibada hii inatarajiwa kuongozwa na Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia, Poland.

Baba Mtakatifu katika salam za rambi rambi anamtaja Marehemu Kardinali Korec kuwa ni mchungaji mahiri, mkarimu na mwaminifu, ambaye katika maisha na utume wake ndani ya Kanisa amejitahidi kuwa ni shuhuda wa Injili na mtetezi wa imani ya Kikristo pamoja na haki msingi za binadamu. Alikamatawa mara kadhaa na kfungwa gerezani, akazuiliwa kutekeleza utume wa Kikasisi, lakini hakukata tamaa, bali akaendelea kuonesha ushuhuda wa nguvu na imani iliyokuwa inabubujika kutoka katika undani wa maisha yake. Ni kiongozi wa Kanisa aliyeshuhudia pia uaminifu wake kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuliwezesha Kanisa kupata Padre na Askofu mahiri wa Injili. Anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kumpokea katika furaha ya uzima wa milele, baada ya mateso na mahangaiko mengi hapa duniani. Baba Mtakatifu anapenda wakuwafariki wote walioguswa na msiba huu mzito pamoja na kuwapatia baraka zake za kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.