2015-10-27 10:53:00

Zingatieni: Sheria, kanuni na taratibu zilizopo wakati huu wa kipindi cha mpito!


Baraza la Makardinali lililoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako tarehe 28 Septemba 2013 lilipewa dhamana ya kutoa ushauri kuhusu marekebisho makubwa yanayopaswa kufanywa kwenye Sekretarieti ya Vatican kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio yaliyokuwa yametolewa na Makardinali katika vikao vyao elekezi. Mageuzi haya tayari yameanza kufanyiwa kazi na Baba Mtakatifu kwa kuunda Sekretarieti kadhaa na utekelezaji wa ushauri wa Makardinali unaendelea kufanyiwa kazi.

Katika kipindi hiki cha mpito kinachoshuhudia mabadiliko makubwa ndani ya Vatican, sheria, taratibu na kanuni zilizotolewa kwenye Katiba ya Kitume, Pastor Bonus zinapaswa kuheshimiwa na kufuatwa kikamilifu. Haya yamo kwenye barua ambayo Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, akimtaka kuhakikisha kwamba, sheria, taratibu na kanuni zinazingatiwa na kuheshimiwa. Wafanyakazi pamoja na wadau mbali mbali wanapaswa kupewa haki zao msingi kama inavyobainishwa kwenye nyaraka mbali mbali za utumishi wa walei ndani ya mji wa Vatican.

Uhamisho na ajira mpya hazina budi kufuata taratibu zilizowekwa na Vatican, daima kwa kushirikiana na Sekretarieti kuu ya Vatican. Taratibu, zote hizi zinagusa vitengo pamoja na taasisi zote zilizoko chini ya Vatican isipokuwa Benki ya Vatican, IOR. Baba Mtakatifu anamtaka Kardinali Parolin kuhakikisha kwamba, ujumbe huu unawafikia wakuu na viongozi wote wenye dhamana mbali mbali katika mji wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.