2015-10-29 15:07:00

Mungu ni upendo, kumbatieni upendo huu kwa kukimbilia ulinzi wake!


Wakristo wanahakikishiwa kupata ushindi kwa vile Mwenyezi Mungu yuko upande wao, hali inayoonesha ukuu, huruma na upendo wake unaomwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Hii ni zawadi ambayo iko mikononi mwa waamini kiasi hata cha kuweza kuthubutu kushangilia ushindi huu, kwani wamefungamanishwa na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Yesu Kristo, Bwana na Mwalimu. Waamini wanawezeshwa kupata ushindi dhidi ya dhambi, ikiwa kama wataambatana na Yesu mwenyewe aliye njia, ukweli na uzima na kwamba, hakuna jambo lolote linaloweza kuwatenga na upendo huu wa Mungu katika maisha yao!

Hii ndiyo zawadi ambayo Mtume Paulo ameiona kwa Wakristo alipokuwa anaandika Waraka kwa Warumi, kwani kwa njia ya Kristo wamezaliwa upya na hivyo kuonjeshwa upendo wa Mungu ambao si rahisi sana kuufafanua kwa lugha ya kibinadamu. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican Siku ya Alhamisi tarehe 29 Oktoba 2015.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni zawadi ambayo mtu anaweza kuikubali na kuipokea au kuitema na kuikataa. Upendo wa Mungu daima utamwambata mwanadamu ambaye ana jukumu la kuupokea na kuumwilisha. Yesu katika Injili aliulilia mji wa Yerusalemu ambao umekuwa ni chanzo cha dhuluma na mateso mengi kwa Manabii kwani watu wake hawakuweza kuupokea upendo huu ambao Yesu anaufananisha na kuku aliyetamani kuwakusanya vifaranga chini ya mbawa zake lakini hawakutaka.

Mwenyezi Mungu daima anapenda na wala hawezi kwenda kinyume cha asili yake kwani Mungu kwa asili ni upendo. Mwanadamu anaweza kuukataa upendo wa Mungu katika maisha yake, lakini anapotubu na kumwongokea Mungu anakirimiwa maisha ya uzima wa milele kama yule Mwizi pale Msalabani. Hiki ni kielelezo cha nguvu ya Mungu, mweza wa yote. Mwenyezi Mungu anaendelea kumlilia mtoto wake anapokimbia upendo wake kwa kutenda dhambi! Mungu haukumu, anaendelea kusubiri kwa hamu kwani anapenda na kuokoa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.