2015-11-11 08:26:00

Papa akutana na kusali na wagonjwa; apata chakula cha mchana na maskini!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa Jimbo kuu la Firenze, Jumanne asubuhi tarehe 10 Novemba 2015 alikazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa Kanisa Katoliki nchini Italia: kujikita katika unyenyekevu na heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu; kujenga na kudumisha umoja na udugu bila ya kujibakiza; kulinda na kutunza mazingira; kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kumwilisha na kudumisha mwelekeo wa kisinodi pamoja na kutekeleza kwa dhati kabisa Waraka wake wa Injili ya furaha katika maisha na utume wa Kanisa.

Wachunguzi wa mambo wanasema, hii ni hotuba ndefu kabisa kuwahi kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Maaskofu wa Italia na itaendelea kuwa ni dira na mwongozo wa Kanisa Katoliki nchini Italia katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mchana akiwa kwenye Kanisa kuu la “Santissima Annunziata” Jimbo kuu la Firenze, aliweza kukutana, kusali na kuongea na wagonjwa pamoja na walemavu 33 mmoja mmoja, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Kanisa kwa watu wake. Wagonjwa na walemavu hawa wamefurahia uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko.

Tukio ambalo limeacha mvuto wa pekee ni kwa maskini na wale “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” walipokutana na kula chakula cha mchana pamoja na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kichungaji Jimbo kuu la Firenze kupitia Jimbo Katoliki la Prato. Maskini hawa walifurahi zaidi wapokuwa wanahudumiwa na Baba Mtakatifu mwenyewe wakati wa chakula kwani daima anasema, maskini ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu Francisko alijipanga mstari na kupokea kadi ya chakula kama maskini wengine wote na hatimaye kuingia kwenye Ukumbi wa chakula unaoendesha na Shirika la Misaada la Jimbo Kuu la Firenze, Caritas Firenze. Maskini 60 wameshiriki chakula cha mchana pamoja na Baba Mtakatifu kwa kutumia sahani za Plastik kama kawaida. Maskini hawa wamesikika wakisema, kwa hakika Baba Mtakatifu Francisko ni kati mmoja kati yao, kwani kila mtu amepata neno la faraja na kuwasikiliza wote kwa umakini mkubwa, kielelezo cha Baba mwenye huruma, anayeguswa na mahangaiko ya jirani zake.

Hapa watu walikuwa na kiu ya kukaa pamoja kama ndugu katika Kristo! Huu umekuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa watu wanaojisadaka kila siku kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Baba Mtakatifu baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa michezo wa Luigi Franchi, Jimbo kuu la Firenze amelishukuru kwa namna ya pekee Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na waamini katika ujumla wao kwa mapokezi makubwa waliomwonesha na kwamba, yale waliyomtendea ni ushuhuda tosha utakaobaki moyoni mwake daima.

Baba Mtakatifu amewashukuru wafungwa waliojenga Altare iliyotumika kwa ajili ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu na hivyo kumwezesha Yesu Kristo kushuka na kukaa kati ya watu wake kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; tayari waamini kumshuhudia kwa ndugu na jirani zao popte pale walipo. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuwaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.