2015-12-03 07:27:00

Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi cha msamaha na upatanisho!


Maadhimisho ya Mwaka mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu ni kipindi cha msamaha na upatanisho; ni muda wa toba na wongofu wa ndani, changamoto na mwaliko kwa waamini kuonesha upendo unaobubujika kutoka katika sakafu za mioyo yao. Ni maneno yaliyosemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahojiano na Jarida la kila juma “Credere” maalum kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Anasema, walau kila Ijumaa ya mwezi, atajitahidi kuonesha tendo la huruma.

Maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu ni jibu kutoka katika undani wa maisha na utume wake, ili kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa kwa nyakati hizi. Huruma ya Mungu ni dhana ambayo imepembuliwa kwa kina na mapana na Mwenyeheri Paulo VI na Mtakatifu Yohane Paulo II. Hii inatokana na ukweli kwamba, ulimwengu mamboleo una kiu ya upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu.

Habari za vita, majanga na mambo ya kusikitisha ndiyo yanayotawala sehemu kubwa ya taarifa zinazotolewa kwenye vyombo vya habari; matukio ambayo ni kashfa kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa changamoto zote hizi, ulimwengu una haja ya kutambua kwamba ukatili na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia si njia muafaka ya kuendelea kuendekezwa, watu wanapaswa kubadilika na kuwa wema zaidi!

Hii ni changamoto hata kwa Kanisa ambalo wakati mwingine limekuwa na msimamo mkali unaojikita katika kanuni maadili, kiasi cha kuwaacha waamini wengi wakiwa wanateseka na utupu wa maisha ya kiroho. Kanisa linapaswa kuwa ni hospitali katika uwanja wa vita; mahali ambapo majeruhi wanatibiwa na kuoneshwa upendo wa dhati. Vita na kinzani za kijamii ni matunda ya biashara haramu ya silaha inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia; ni biashara inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu; yote haya ni matukio dhidi ya ubinadamu, ndiyo maana Jubilei ya huruma ya Mungu ni mwaliko kwa wafanyabiashara kama hawa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu tayari kuanza hija mpya ya maisha.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, ni mdhambi ndiyo maana kila baada ya siku kumi na tano anakimbilia huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho. Baba Mtakatifu anakumbuka vyema kabisa kwamba, akiwa na umri wa miaka kumi na saba kunako tarehe 21 Septemba 1953 alisikia wito wa kuwa Padre, baada ya kuonja huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho. Hii ni Sakramenti aliyopewa na Padre Carlos Benito Duarte Ibarra. Kanisa linapoadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Mathayo, daima anakumbuka maneno ya Yesu, aliyemwangalia Mathayo mtoza ushuru kwa jicho la upendo, akamchagua.

Na hii ndiyo kauli mbiu ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameitumia kama Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro, “Miserando atque eligendo”. Hapa Yesu alimwonea huruma Mathayo, akampenda na kumchagua ili aweze kuwa ni chombo cha huruma ya Mungu kwa waja wake. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo yanayomwonesha kuwa ni Baba na Mama, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuambata huruma, upendo na uvumilivu kwa jirani zao. Haya ni mambo msingi ambayo yaliibuliwa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya watawa iliyoadhimishwa kunako mwaka 1994. Hata leo hii kuna haja ya kuendeleza mchakato wa huruma na upendo wa Mungu kati ya watu, ili kuambata haki na amani.

Waajiri wanapaswa kuwa na huruma na upendo kwa wafanyakazi wao kwa kuwapatia haki zao msingi, utambulisho; kwa kuwawekea akiba ya uzeeni na hifadhi za kijamii, vinginevyo mwajiri anawatumia wafanyakazi kama chombo cha kuzalisha mali pasi na huruma wala mapendo. Kumbe mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni nafasi kubwa ya kuonesha huruma na mapendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu anahitimisha mahojiano maalum na Jarida la “Credere” kwa kusema kwamba, kila Ijumaa moja ya mwezi atashuhudia huruma ya Mungu, kielelezo cha upendo wa Mungu kama ambavyo wanafanya wazazi kwa watoto wao wadogo, ili kuonesha kwamba, kweli wanawapenda kwa dhati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.