2015-12-07 07:44:00

Si rahisi kusamehe na kusahau majanga yanayowaandama wakimbizi!


Yesu Kristo daima anasafiri pamoja na waja wake wakati wa raha, furaha na majonzi. Kuna maelfu ya watu ambao amefariki dunia wakiwa njiani kutafuta usalama na nafuu ya maisha, wao sasa wako mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Lakini ikumbukwe kwamba, Yesu Kristo alikuja ulimwenguni ili kumpatia mwanadamu matumaini ambayo yanapaswa kumwambata mwanadamu katika maisha yake pasi na kukata tamaa.

Yesu Kristo ana nguvu zaidi kuliko kifo na hata nguvu za giza. Amekuja ulimwengu ili kuwashirikisha walimwengu Injili ya huruma ya Mungu. Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoyatoa Jumapili tarehe 6 Desemba 2015 wakati alipokuwa anawasha taa kwenye Pango la Noeli kwa Mwaka 2015 huko Assisi. Noeli ya Mwaka huu sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu iwe ni fursa kwa waamini kufungua nyoyo zao kwa huruma ya Mungu na msamaha, lakini Baba Mtakatifu anakaza kusema, si rahisi sana kutoa msamaha hasa kutokana na majanga yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu ameyasema hayo kwani ndani ya Pango la Mtoto Yesu kwa mwaka huu wameweka mashua ya wakimbizi na wahamiaji waliokufa maji wakitafuta usalama na nafuu ya maisha Barani Ulaya. Baba Mtakatifu anawapongeza wanajeshi wa vikosi vya maji kwa kazi kubwa wanayotenda na kwamba, wao wamekuwa kweli ni vyombo vya matumaini yanayoletwa na Kristo Yesu. Wao wamekuwa ni cheche za matumaini kwa watu waliokata tamaa. Anawashukuru pia wananchi wa Italia, lakini kwa namna ya pekee Kusini mwa Italia ambao wamekuwa ni kielelezo cha upendo na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji wanaoingia kila kukicha nchini Italia.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wale wote watakaotembelea Pango la Mtoto Yesu wataguswa na ukarimu kiasi cha kusema kwamba, hata mimi nimekuwa ni mbegu ya matumaini kwa wale waliokata tamaa. Baba Mtakatifu anapenda kuwaambia wakimbizi na wahamiaji popote pale walipo wainue vichwa vyao kwani Bwana yu karibu kuja na anabeba ndani mwake nguvu, wokovu na matumaini, wanaweza kuwa na majonzi mioyoni, lakini wawe na matumaini makubwa kwa Kristo Yesu anayezaliwa tena kati yao. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia wote heri na baraka ya Siku kuu ya Noeli ambayo kwa mwaka huu inaadhimishwa sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.