2015-12-11 08:17:00

Mkitubu na kuongoka, mtapata chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha!


Nyoka ni hayawani anayetisha kutokana na sumu yake inayofisha. Nyoka ni ishara ya chuki, wivu, ubaya, hila, ufisadi, ujanja, ubinafsi, ukali, uonevu. Kila anapoonekana hupigwa na kuuawa. Kulikuwa na mtawala mmoja Afrika aliyepachikwa jina la “nduli nyoka” kwa sababu alivamia kwa nguvu ardhi ya nchi jirani na kuwatendea kila uovu raia wa sehemu hiyo. Nchi iliyovamiwa ikaingiwa na woga mkali na ikatangaza vita vya kumpiga nyoka huyo. Baada ya kumpiga na kumfukuza wananchi wakawa huru na kufurahi sana.

Leo ni dominika ya tatu ya Kipindi cha Majilio iitwayo dominika ya furahini. Lakini katika Injili ya leo haioneshi furaha kwani John au Yohane mbatizaji anatumia lugha kali kwa wale waliomfikia. Anawaita kuwa ni “Wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kukimbia hasira itakayokuja?” Lk 3:7-8). Nyoka hao wenye sumu inayoua au kama usaha wa jipu linalouma, ni nguvu hasi zilizo nafsini na zinamnyima mtu furaha katika maisha. Sumu na usaha huo vikiondolewa mgonjwa anapona na kufurahi. Kuondoa nyoka hao ndiyo kubadilika ambako kwa kigiriki ni metanoia. Kubadilika au wongofu ni ujumbe tunaopata leo toka kwa Yohane Mbatizaji. Fikra zetu zisipobadilika, Mungu hawezi kuingia katika maisha yetu.

Watu wanaogopa mabadilio aletayo Kristo na hivi wanatumia njia nyingi na vikwazo vya kumzuia asiingie mioyoni mwetu. Namna mojawapo ya kumzuia ni kujitetea na kuhoji maswali mengi, kwa nini, mbona, kama, endapo akifika, yaani. Hayo yote yanalenga kumzuia asifike kusudi tuweze kuendelea na ufisadi tuliouzoea. Namna nyingine ya kukataa mabadiliko hasa kwa watu wa dini ni ile ya kutunga ibada ya pekee ya kuabudu au kuwa na ukarismatiki unaokutuliza dhamiri kusudi nyoka aendelee kutulia ndani mwetu.  Wongofu anaopendekeza Yohane leo, siyo ule tuliozoea kuusikia, yaani kuacha dhambi ya kuua, ya kuzini, ya kusema uwongo, ya kuiba, la hasha bali ni wongofu wa kuacha dhambi ya “kutotimiza wajibu.” Dhambi hiyo tunaiona katika makundi matatu yanayomjia Yohane Mbatizaji na kumwuliza swali linalolingana. “Tufanye nini?” Hata sisi tunaojiandaa kusherekea sikukuu ya Noeli tunaweza kuungana na makundi hayo kumwuliza Yohane Mbatizaji “Tufanye nini?”

Kundi la kwanza ni makutano ya watu wanauliza: “Tufanye nini basi?” Yohane anawajibu bila kuzunguka wala kupindisha mambo “Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo.” Mavazi na chakula ni mahitaji muhimu ya binadamu. Kwa hiyo alama ya kwanza ya wongofu unaomfungulia Yesu mlango aingie katika maisha yetu ni kugawa mahitaji ya lazima kwa wasio nayo. Wazo la Mlango ni muhimu sana wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Huu ni mlango wa huruma inayomwilishwa katika upendo! Kwa hiyo kuwa mbinafsi, mchoyo, bahili yaani mkono wa bikira, mbadhilifu, mlimbikizaji wa raslimali ya umma kwa ujanja ni dhambi ya “kutotimiza wajibu.”

Dhambi hii anaisema pia mtume Yakobo: “Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi” (Yak 4:17). Kadhalika watu wachache sana wanaiungama dhambi hii ya mahusiano ya kimaadili kwa sababu hatuoni umuhimu wa kufanya mema. Anahoji Mwinjili Yohane katika barua yake ya kwanza: “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, Je, upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo? Ndugu zangu tusipende kwa neno, wala kwa ulimi bali kwa tendo na kweli.” (I Yoh. 3:17-18). Yohane Mbatizaji anataka kuunda jumuia mpya inayotawaliwa na ufalme wa Mungu kinyume cha jamii ile ya kibinafsi. Aidha anatufundisha kuridhika na maisha ya kawaida. Yeye aliyevaa ngozi ya ngamia na kuponea asali na nzige, anafundisha msamiati mpya wa upendo ambao ni wa kutoa. Jumuiya ya Mungu yenye haki ni ile ambayo wote wanagawana sawa mali ya ulimwengu huu na wanaishi kwa furaha kwani sisi sote ni ndugu wa baba mmoja. Mtu anakuwa na furaha ya kweli anapowapa furaha wahitaji.

Kundi la pili ni watoza ushuru wakamwuliza: “Mwalimu tufanye nini sisi?” Watoza ushuru walikuwa wala rushwa na mafisadi wa kutisha sana. Walitoza kodi na ushuru mkubwa na kiasi kinono kilingiia mifukoni mwao, hawa walikula sahanani moja na wafanyabiashara waliokuwa wanakwepa kulipa kodi halali kwa kutoa kitu kidogo!. Hapa Yohane hawaambii wabadili shughuli, la hasha, kwa sababu kodi zinahitajika kwa ajili ya kuendesha huduma za jamii, bali anawaangalisha: “Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoambiwa.” Kumbe, ufisadi na rushwa ni dhambi kubwa na jamii inaonywa kubadilika. Viongozi wa serikali na dini wanaonywa kujiepusha na dhambi ya kujilimbikizia mali, kwani watashindwa kuonesha mfano na kutoa ushahidi wa uaminifu kwa raia na waamini wanaowaongoza. Watu wanataka kuona ushuhuda unaojikita katika uhalisia wa maisha, longo longo kibao hazina nafasi tena, yaani hapa tungeweza kusema kwa ujasiri tu, hapa kazi tu baba!

Kundi la tatu ni la askari wakamwuliza: “Sisi nasi tufanye nini?” Yohn anawadai mambo matatu: Mosi “Msidhulumu mtu,” neno la Kigiriki lililotumika hapa ni diaseichte maana yake kutisha na kutetemesha kumbe wanaambiwa, “msimtetemeshe mtu.” Kwa vile askari wana silaha ipo hatari ya kuwatisha wanyonge na kuwapokonya mali zao. Pili, “msishtaki kwa uongo,” yaani kutowabambatikiza watu kesi za uwongo ili kupata mshiko. Tatu, “mtoshewe na mshahara wenu.” Kwa hiyo askari wasitumie silaha (nguvu) ili kuwatisha wanyonge ili kupata fedha, bali watumie nguvu zao vizuri na kutetea haki, amani na maridhiano ya kijamii.

Yohane Mbatizaji anaendelea kutumia lugha kali zaidi anaposema: “yuaja mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.” (Lk. 3:17) Tafsiri ya moto uounguza wadhambi inatofautiana kabisa na hitimisho la Yohane Mbatizaji linalotupeleka kwenye furaha ya leo isemayo: “Basi, kwa maonyo mengine mengi aliwahubiri watu.” Hapa neno maonyo limefasiriwa vibaya kutoka kigiriki euEggelizeto lenye maana ya ujumbe mzuri, ujumbe unaotuliza, Injili au Habari njema, Breaking news!

ivi “Kwa ujumbe mwingi mzuri wa kutuliza Yohane Mbatizaji aliwahubiria watu.” Huu ni ujumbe mzuri wa kutuliza, ni maneno ya furaha na faraja kwani makapi hayo ni ubaya ulio ndani ya kila mtu huo utapeperushwa na upepo utakaofika. Upepo huo unakumbusha Roho Mtakatifu Pentekoste afikaye kwa upepo mkali na kuleta nguvu mpya inayopuliza makapi yaliyo ndani ya mtu, itayapeperusha makapi yaliyo ndani ya nyumba, ndani ya familia, ndani ya jamii, ndani ya taifa nk. Unapofika moto wa hasira ya Mungu, upepo unaopepeta, hapo kutakuwa na furaha na matumaini kwani sasa nyoka watatoroka, makapi yatapeperushwa, majipu yatatumbuliwa, uovu, madhulumu, ukandamizaji, ufisadi, rushwa, uchakachuaji hivi vyote vitapeperushwa na upepo mkali wa Roho ya Mungu.

Yesu anafika wakati wa Noeli na kuunguza kila uovu. Tunategemewa kuupokea na kuuenzi moto ambao ni Kristu na upepo ambao ni Roho mtakatifu atakayetumwa naye. Kwa vyovyote hatutegemei mabadiliko ya mara moja, lakini kama kila mmoja ajaribu kufungua moyo kadiri ya maelezo anayotupendekezea Yohane Mbatizaji hapo jamii yetu itabadilika (itaongoka) na ulimwengu utakuwa mpya na upendo na huruma ya Mungu inaweza kutawala katika mioyo na akili za watu! Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu kwa kuachana na dhambi tunazozitenda kwa: mawazo, maneno, kwa vitendo na hasa kwa kutotimiza wajibu, changamoto inayotolewa na Yohane Mbatizaji katika Injili ya Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.