2015-12-18 09:02:00

Wanasiasa kiteni maisha yenu katika: Weledi, uaminifu, ukweli, uwazi na uadilifu


Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika mahubiri yake kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa wabunge nchini Italia, hivi karibuni, amewataka wabunge hao kutekeleza dhamana na wito wao kwa kujikita katika weledi, uaminifu, ukweli, uwazi, uadilifu na sadaka kwa ajili ya huduma kwa wananchi waliowachagua nchini Italia. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linawataka wanasiasa kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira hususan mingoni mwa vijana ambao wanaendelea kukata tamaa.

Wanasiasa wanakumbushwa kwamba, siasa kimsingi inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma makini kwa wananchi, vinginevyo wananchi watakosa imani kwa wabunge wanaowawakilisha ikiwa kama watakuwa Bungeni kwa ajili ya kujitafuta na kutafuta mafao yao binafsi. Mwelekeo wa namna ya hii ni hatari kwa Serikali na Bunge, mihimi mikuu ya dola inayopaswa kuonesha weledi, tija na huduma makini kwa wananchi wake. Pango la mtoto Yesu ni alama ya unyenyekevu, amani, udugu na mshikamano, mambo ambayo yanapaswa kutawala hata miongoni mwa wanasiasa.

Fadhila ya unyenyekevu katika huduma ina mavuto na mashiko kwa wengi, kinyume kabisa cha ubabe na uchu wa madaraka unaooneshwa na baadhi ya viongozi wanaochaguliwa na wananchi. Uongozi ni huduma hasa kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na wala si ujiko kwa mtu awaye yote! Wanasiasa na viongozi wa Serikali wanapaswa kuwa makini ili kuangalia shida, changamoto na magumu yanayowakabili watu wao, tayari kutafuta mbinu mkakati wa kupambana na hali kama hizi, ili kuwajengea wananchi imani na matumaini kwa viongozi wao wa kisiasa.

Wanasiasa ni watu wanaopaswa kusimama kidete kulinda, kutafuta na kudumisha mafao na ustawi wa wengi badala ya kugubikwa na ubinafsi, uchoyo na uchu wa mali na madaraka. Wanasiasa ili waweze kuheshimika na kuthaminiwa na wananchi wajitahidi kuwa ni mashuhuda wa ukweli, haki na amani. Mafao ya wengi anakaza kusema Kardinali Bagnasco yanajionesha kwa njia ya fursa za ajira, hususan miongoni mwa vijana wa kizazi kipya; ili kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Kardinali Bagnasco anasema, kuna dalili za kukua kwa uchumi nchini Italia pamoja na ongezeko la fursa za ajira kwa vijana, lakini bado kuna kundi kubwa la vijana wasiokuwa na fursa za ajira, hali ambayo inawajengea hofu ya kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, jambo ambalo linaendelea kuwadumaza. Ni matumaini ya Kardinali Bagnasco kwamba, mwaka 2016 utakuwa ni mwaka wa matumaini na ukuaji wa uchumi nchini Italia, baada ya kusua sua kwa muda wa miaka mingi kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.