2015-12-26 08:58:00

Sakata la Familia Takatifu! Sipati picha!


Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, punde tu baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia na mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Mababa wa Sinodi walikita majadiliano, sala na tafakari zao kuhusu matatizo, changamoto na fursa zilizopo katika familia, ili kutekeleza wito na utume wake katika Kanisa na ulimwengu mamboleo! Changamoto hizi zimeikumba pia Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu! Ukitaka kusutwa kwa umbea sikiliza sakata hili!

Wazazi wengi wanashtuka sana wanapowaona watoto waliowazaa na kuwalea kwa maadili mazuri ya tamaduni, mila, desturi njema na dini kimila dini yao, wakikengeuka na kuishi kinyume cha maadili waliyowapatia. Mara nyingi wazazi hao wanakata tamaa na wanajilaani na kujisemea: “kuzaa ni kuondoa maradhi.” Wazazi wengine hawaelewi maana yake, lakini wanatulia na kuwaombea watoto. Leo tutaushuhudia mzozo uliojiri katika familia moja, ambapo mtoto anatenda mambo kinyume cha mila na desturi za wazazi wake. Anapoulizwa kisa na maana, anawarushia maneno yasiyoeleweka mbele ya watu.

Ili kufaidika na sakata hilo, tufuatilie kwanza mazingira ya Injili ya leo. Mwinjili Luka anaanza fasuli hii kwa maneno haya: “Wazazi wa Yesu.” Sisi tunaelewa kwamba, wazazi wa Yesu walikuwa Yosefu na Maria, lakini Mwinjili anasema tu kifupi “wazazi wa Yesu.” Lengo ni kuonesha kwamba sakata hilo linawahusu wazazi wote, hasahasa wazazi wa taifa la Waisraeli. Wazazi hawa pamoja na ndugu na jamaa walikuwa na utamaduni wa kwenda kila mwaka kula sikukuu Yerusalemu kama inavyosemwa: “Wazazi wa Yesu walienda kila mwaka Yerusalemu kwenye sikukuu.” Safari hii walipoenda Yesu alikuwa na miaka kumi na miwili. Wakati wa kurudi  Mtoto Yesu alibaki Yerusalemu bila kutaarifu, nao wazazi walipanganika bila kuhakikisha mtoto wao yuko wapi.

Kwa hiyo, kama simulizi hili ni la kihistoria, basi hapa inachanganya na kuleta wasiwasi, hasa kitendo cha Yesu kutotaarifu wazazi ni utovu wa nidhamu usiostahili kuigwa. Wazazi wanapogutuka kwamba wamepotezana maboya na mtoto wao, wanaanza kumtafuta kati ya ndugu na jamaa kwa siku tatu bila mafanikio! Taabu kweli kweli! Eti Waswahili wanakaza kusema, uchungu wa mwana anaujua mzazi! Wanarudi Yerusalemu na kumkuta mtoto Hekaluni ameketi kati ya Makuhani akiwasikiliza na kuwahoji maswali; akiwapatia nondo za nguvu, kiasi cha wao kushika tama! Mama yake anajitosa kumhoji mtoto wake, ndipo Yesu anarudisha kibao na kuwagombeza wazazi wake.

Hebu tuendelee kulitafakari sakata hili na kugundua sababu za Yesu kubaki Yerusalemu bila kuwataarifu wazazi wake, na kwa nini wazazi wenyewe wasigundue hilo kabla. Hapa ni dhahiri tupo katika fasuli ya kitaalimugu. Sakata zima limejengwa katika mazingira ya sikukuu Pasaka ambapo wazazi wa Yesu walienda kila mwaka Yerusalemu kusherehekea Sikukuu. Hapa unaona waziwazi kwamba Familia ya Yesu ni ya Kiyahudi kwelikweli inayoshikilia: mila, utamaduni na taratibu za dini, yaani kwenda kuhiji na kusali Yerusalemu kila mwaka.  Kwa hiyo, hii ni Familia ya mfano wanaoshika mila na desturi za dini na za taifa na wanajitahidi kutaka kurithisha mila hiyo kwa watoto wao. Hapa hayatajwi majina ya Yosefu na Maria kwa sababu hii ni familia ya mapokeo ya kimila na utamaduni wa kiyahudi inayofuata kinaganaga utamaduni wake wa kila mwaka kwenda Yerusalemu na kurudi.

Wazazi walitegemea kwamba Yesu angefuata mfumo wa safari ya utamaduni wa wazazi wake kumbe, anafanya kinyume. Kitendo anachofanya Yesu kinaonesha kuwa utamaduni wa jamii ya Wayahudi umevamiwa. Kwa hiyo jamii kwa niaba ya mama, inaingia kwenye mjadala  mkali na Yesu aliyejitenga na mapokeo hayo. Fasuli inaeleza kuwa wazazi “walimtafuta kati ya ndugu na jamaa, na wajuani bila mafanikio.” Hivi Yesu hafuati wazazi, wala jamaa. Kumbe, yatakiwa wazazi wamfuate yeye aliko na msimamo wake. Ukweli huo unauona kwenye taarifa anayotoa Malaika kwa Zakaria kwamba Yohane ataongozwa na moyo na akili ya Baba dhidi ya watoto, kwamba Agano la kale lipokee Agano Jipya na wala siyo kinyume chake.

Halafu yasemwa tena kwamba “Yesu alikutwa ameketi Hekaluni kati ya Makuhani na Marabi.” Kwa kawaida ni Rabi peke yake ndiye aliyekuwa anaketi anapofundisha na wasikilizaji wake husimama. Kwa hiyo hapa Makuhani na Marabi walikuwa wamesimama wakimshangaa ”Existemi” kwa Kigiriki maana yake kushtuka, kuchukizwa kwa sababu Yesu alitoa maelezo au tafsiri ya Maandiko tofauti na walivyozoea kutoa  wao. Nao wazazi wake wafikapo wanashangaa, ”exploesim” kwa Kigiriki maana yake kushangaa kwa kutoelewa. Hawakuelewa kabisa maana ya kitendo cha mtoto wao kubaki Yerusalemu bila kuwataarifu. Familia ya Yosef na Maria inaona kuwa jambo hili ni jipya, lakini wanalipokea na kutaka kulijadili. Hapa tunafundishwa kutambua kuwa pale itokeapo watu wote wanashikilia mila na desturi zao kiaminifu na hawataki kubadilika, na kuna wengine hawaelewi na kushangaa, lakini wanaacha nafasi ya kujadiliana na kupokea ukweli mpya kama hii familia ya Maria na Yosefu.

Tamko la Mama kwa Yesu ni  “Mwanangu.” Tamko hili halimwakilishi Maria, bali linamwakilisha Mama wa taifa zima la Waisraeli anayemwuliza mtoto wake. Mama huyo angeweza kuuliza hivi: “Mwanangu kwa nini umefanya hivi, mimi silielewi fumbo hili la Masiha wa Mungu. Tulikuwa tunasubiri Masiha lakini siyo kama huyu aliyejionesha Yesu kwenye Pasaka.” Kisha Yesu anafungua mdomo kwa mara ya kwanza katika maisha yake, na anasema: “Kwa nini mlinitafuta?” Kama vile angetaka kusema: “tusijuane, hebu mnitue,” na kuendelea “hamkujua kwamba inabidi nishughulike na mambo ya Baba yangu.” Kumbe, Yesu ni Mwana ambaye Baba anaridhika naye, naye mtoto hana budi kumtii Baba yake kwanza, yaani afuate matakwa ya Baba. Kwa hiyo mama ya Waisraeli budi atambue na afungue moyo kupokea matakwa ya Bwana. Kwamba Yesu amefika kufundisha kuwa Mungu ni Aba!Baba wa wote!

Hapa familia zetu zinapata ujumbe kwamba, mtoto yeyote yule anapokuwa wakubwa yabidi wazazi wamwache afuate maisha yake. Ndivyo anavyomaanisha Yesu anapowahoja wazazi wake: “Hamkujua kwamba maana ya maisha yangu siyo kubaki nyumbani bali kufanya utume, kushika majukumu yangu ya maisha. Inabidi wazazi watambue wito ambao Mungu anamtakia mwana wao. Aidha, wazazi wanatakiwa wapokee mabadiliko hasa ya kutengana na mwana wao katika kipindi hicho cha kuachana naye hasa pale mwana wao anapopokea majukumu mazuri ya mahusiano ya mapendo. Daima warekebishe maisha kuendana na maisha mapya yanayoonekana katika mtoto wao. Wajiweke katika mazingira mapya, vingine hawawezi kuwa na mahusiano yatakiwayo na mtoto wao.

Yasemwa pia kuwa “Baba na mama hawakuelewa maneno ya mwana.” Hii siyo mara ya kwanza hawakuelewa, kwani hata maneno ya Simeoni hawakuyaelewa. Lakini “mama alitunza yote katika moyo wake.” Kwamba Maria hata kama hakumwelewa mwanae asiyefuata utamaduni wao, lakini bado wanamwamini tu. Mapato yake “Yesu akajiweka chini ya wazazi.” Hivi ndivyo wanavyoweza kukua sawasawa na kuwa na hekima wakijiweka chini ya wengine na kutaka kujifunza jinsi ya kutumikiana vyema. Heri kwa siku kuu ya Familia Takatifu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.