2015-12-31 07:15:00

Familia washeni moto wa mapendo, kushuhudia Injili ya familia!


Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, hapo tarehe 27 Desemba 2015, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amewakumbusha waamini wa Parokia ya “Santissima Trinità, huko Schio, Italia kwamba, si rahisi kupata familia iliyo kamilifu hapa duniani, lakini hii si sababu msingi ya kuwakatisha wanafamilia kutojikita katika mchakato wa ukamilifu wa maisha ya ndoa na familia, kwa kujifunza kuishi na kusaidiana kikamilifu kadiri ya mazingira ya kila familia.

Kardinali Parolin anakaza kusema, familia haina budi kuwa wazi kupokea na kumwilisha fadhila ya: msamaha, upendo na ukarimu katika hija ya maisha yake ya kila siku. Waamini wanaendelea kuhamasishwa na Mama Kanisa ili kuhakikisha kwamba, wanafungua malango ya maisha yao, ili kweli huruma na upendo wa Mungu uweze kukita mizizi yake, tayari kushuhudia Injili ya familia inayosimikwa katika sadaka, majitoleo pamoja na kufanya maamuzi magumu katika maisha, ili familia iweze kustawi na kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani utakatifu wa maisha.

Kardinali Parolin anasema, Mwenyezi Mungu ameonesha upendo na mshikamano wa dhati na binadamu kwa kuamua kuja duniani, akazaliwa na kulelewa katika familia, iliyokuwa wazi kuambata huruma na upendo wa Mungu, mambo msingi anayokazia Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Lakini ikumbukwe kwamba, Fumbo la Umwilisho linapata ukamilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, kumbe hata katika familia kuna Misalaba ya maisha inayopaswa kubebwa kwa imani na matumaini

Mateso na ufufuko ni pande mbili za Fumbo la upendo katika maisha ya mwamini, kwani kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Yesu ameonesha upendo wa hali ya juu kabisa kwa binadamu kwa kuyamimina maisha yake ili yawe ni fidia kwa wengi. Fumbo la Msalaba ni mahali pa kujifunza kupenda na kupendwa, mchakato unaoambata hija ya maisha ya mwanadamu na kwamba, hii ndiyo ile ndoto ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuiona inatekelezwa katika maisha ya binadamu.

Mwenyezi Mungu anataka kuunda familia na kuitegemeza ndiyo maana Mama Kanisa katika kipindi cha miaka miwili ameadhimisha Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, lengo ni kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, licha ya vyombo vya habari kutia chumvi nyingi kiasi hata cha kutaka kuharibu mchuzi! Injili ya familia ina uzuri na changamoto zake, lakini Kristo Yesu, anataka kuendelea kuwa ni Msamaria mwema anayeganga na kuponya madonda ya familia zinazomlilia kwa imani na matumaini kwa njia ya Kanisa lake.

Kardinali Parolin anakaza kusema, familia zinapaswa kuwasha moto wa mapendo kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, lakini zaidi kwa toba na msamaha, kwa kutambua kwamba, familia ni shule ya upendo, ukarimu, amani na huruma. Amewataka viongozi wa Parokia kuwasaidia wanafamilia kushuhudia Injili ya familia kwa kujisikia kuwa kweli ni sehemu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa mahalia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.