2016-01-07 09:03:00

Changamoto za kimaadili zinazowakabili wafanyabiashara!


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, tarehe 6 Januari 2016 ametoa mhadhara kwenye mkutano wa kimataifa unaofanyika kwenye Chuo kikuu cha De Los Andes, nchini Chile kuhusu changamoto za kimaadili zinazowakabili wafanyabiashara katika ulimwengu mamboleo, wakitambua kwamba, kama viongozi wa masuala ya biashara wanapaswa kuwa makini kwani huu ni wito wao katika Jamii inayowazunguka. Mkutano huu umefunguliwa rasmi hapo tarehe 5 na unahitimishwa, tarehe 7 Januari 2015.

Ikumbukwe kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anakazia kanuni maadili, utu wema pamoja na kuwajali maskini katika sera na mchakato wa maendeleo ya binadamu na kamwe faida kubwa isiwe ni lengo la uzalishaji na utoaji huduma, kwani matokeo yake ni kudhalilisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kazi, makazi, ardhi na chakula ni mambo ambayo yanapaswa kuangaliwa kwa makini, ili yaweze kuwanufaisha watu wengi zaidi anasema Baba Mtakatifu Francisko na kwa njia hii, watu wanaweza kuchangia katika mchakato wa maendeleo ya nchi yao.

Wafanyabiashara wanapaswa kuwa na dira na mwongozo utakaowasaidia kufikia malengo yao, huku wakiwa makini katika utunzaji wa nyumba ya wote, kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote, Laudato si!

Kardinali Turkson katika hotuba yake amefafanua mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na wafanyabiashara ili kuchangia katika ustawi na mafao ya wengi, kwa kuzalisha bidhaa na huduma ambazo ni muhimu na zinahitajika kwa ajili ya binadamu na ustawi wake. Wafanyabiashara hawana budi kuhakikisha kwamba, wanakuza na kudumisha mshikamano na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huduma na bidhaa zinazozalishwa zijitahidi kukidhi mahitaji msingi ya binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini, ili kuhakikisha kwamba, kweli haki inatendeka kwa wote.

Kazi njema zinazozalishwa na wafanyabiashara zinapaswa kusaidia mchakato wa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Hapa mkazo unawekwa kwa namna ya pekee kwa ajili ya sera zinazosaidia kuzalisha fursa za ajira kwa wafanyakazi ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu, kwani kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu. Wafanyabiashara wathubutu kuwekeza katika rasilimali watu ili kuboresha shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma badala ya kukumbatia faida kubwa. Ikumbukwe kwamba, uzalishaji wa fursa za ajira ni sehemu ya mchakato unaochangia kwa kiasi kikubwa utu na heshima ya binadamu.

Kardinali Turkson anakaza kusema, shughuli za biashara na huduma hazina budi kuongozwa na kanuni auni, inayowawezesha wafanyakazi kutumia vyema karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika uzalishaji na utoaji huduma. Wakuu wa kazi watambue kwamba, wafanyakazi wanapaswa kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo ya sehemu zao za kazi.

Hapa kiongozi anapaswa kuambata fadhila ya unyenyekevu, ili kuonesha dira na mwongozo unaopaswa kufuatwa kwa ajili ya maendeleo ya wengi, tayari kuwashirikisha wengine matunda ya kazi ya mikono ya wanadamu. Kwa namna ya pekee kabisa, viongozi wanapaswa kuwa ni watu wanaojali, wanaolinda na kuelekeza, wao wenyewe wakiwa ni mfano bora wa kuigwa na wafanyakazi wengine.

Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani anahitimisha hotuba yake kwa kuwataka viongozi na wafanyabiashara kuwa na huruma na mapendo kwa wafanyakazi wao, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Huruma na kujali, visaidie mchakato wa kukuza na kudumisha kipaji cha ugunduzi, ili kuchangia katika ujenzi wa dunia iliyo bora zaidi kwa kulinda na kuendeleza utunzaji bora wa mazingira ambao una uhusiano mkubwa na ustawi na maendeleo ya binadamu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.