2016-01-07 16:20:00

Matendo ya huruma ni kiini na vinasaba vya maisha ya Kikristo!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Siku ya Alhamisi, tarehe 7 Januari 2016 amesema kwamba, matendo ya kiroho na kimwili ni kiini na vinasaba vya imani ya Kikristo, inayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Waamini wajitahidi kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu pamoja na mambo yanayowapeleka mbali na uso wa Mungu, aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake!

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujifungamanisha na kuendelea kubaki ndani ya Mwenyezi Mungu, huku wakimwambata pia Roho Mtakatifu, tayari kupambanisha Roho Mtakatifu na roho wa uwongo ambao wanapelekea waamini kwenda kinyume cha mapenzi ya Mungu, kama anavyofundisha Mtakatifu Yohane katika nyaraka zake. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa na busara pamoja na hekima ili kufuata na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha ya kila siku huku wakitambua kwamba, hapa duniani kuna wapinga Kristo wanaoendelea kusababisha mateso na mahangaiko ya waamini kiroho na kimwili.

Waamini wakimezwa na malimwengu hapo watambue kwamba, watakuwa mbali na Roho Mtakatifu, anayewajalia neema na baraka za kuendelea kukaa ndani ya Mwenyezi Mungu. Ili kufanikisha azma hii, wanapaswa kwanza kabisa kumtambua Yesu aliyeshuka kutoka mbinguni na kuutwaa ubinadamu na kukaa kati ya watu wake. Roho asiye mtambua Kristo huyo ni mpinga Kristo na wala hatoki kwa Mungu anasema Baba Mtakatifu Francisko. Amri kuu ni kumwamini Mwana wa Mungu Yesu Kristo pamoja na kumwilisha upendo huu kwa jirani na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anakaza kusema Kanisa linaweza kupanga mikakati mingi ya shughuli za kichungaji katika maisha na utume wake, lakini lisiposhikamana na kuambatana na Kristo katika hija ya maisha ya wanadamu, linaweza kujikuta linamezwa na malimwengu! Waamini wajitahidi katika hija ya maisha yao kuhakikisha kwamba wanamwilisha matendo ya huruma katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, kwani upendo kwa jirani ni amri na agizo la Kristo mwenyewe ambaye anajitambulisha kwa wadogo, wanyonge na wale wanaoteseka: kiroho na kimwili.

Roho Mtakatifu anayetoka kwa Mwenyezi Mungu anawakirimia waamini ari na moyo wa sadaka na huduma kwa wale wote wanaohitaji msaada wao. Waamini wawe tayari kujisadaka na kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kuwahudumia, kuwasikiliza na kuwafariji wale wanaohitaji msaada na huduma yao. Hii ndiyo ile njia ambayo imeandaliwa na Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia Roho Mtakatifu, ili wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kuondokana na ubinafsi pamoja na hali ya mtu kujitafuta mwenyewe. Waamini wawe na ujasiri wa kufanya tafakari ya kina ili kufahamu kile kinachotendeka mioyoni mwao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.