2016-02-23 11:37:00

Adhabu ya kifo imepitwa na wakati!


Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye makao yake makuu mjini Roma inaunga mkono juhudi za Baba Mtakatifu Francisko za kutaka Jumuiya ya Kimataifa kufuta adhabu ya kifo kwani imepitwa na wakati. Maoni ya wengi yanaonesha kwamba kuna uwezekano wa kudhibiti uhalifu bila kusababisha mauaji ya wahalifu. Maisha ya binadamu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo inapaswa kuendelezwa na kudumishwa. Baba Mtakatifu anawasihi viongozi Wakatoliki wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kutoridhia utekelezaji wa adhabu ya kifo katika nchi zao.

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Jumatatu tarehe 22 Februari 2016 imeendesha kongamano la kimataifa dhidi ya adhabu ya kifo duniani kwa kuwashirikisha mawaziri wa sheria kutoka katika nchi 30 ili kuridhia mchakato wa kufuta adhabu ya kifo duniani. Kumekuwepo na maendeleo makubwa tangu mwaka 2014, Baraza kuu la Umoja wa Mataifa liliporidhia ufutaji wa adhabu ya kifo. Mongolia na Pwani ya Pembe ni kati ya nchi ambazo zimefuta adhabu ya kifo kutoka katika Sheria za nchi. Wachunguzi wa mambo wanasema mahali ambapo kuna vitendo vya kigaidi, maoni ya wengi ni kuendeleza adhabu ya kifo!

Rais Sergio Mattarella wa Italia akizungumza na mawaziri wa sheria kutoka katika nchi mbali mbali, katika Kongamano lililoandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio anakaza kusema, takwimu zinaonesha kwamba, adhabu ya kifo haijasaidia kupunguza vitendo vya uhalifu na matokeo yake ni jamii kutothamini maisha na utu wa mwanadamu; mambo muhimu yanayojenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano kati ya watu na serikali.

Rais Mattarella anasema, kuna haja ya kuwasaidia wafungwa ili wanapomaliza adhabu zao, waweze kurejea tena katika jamii wakiwa watu wema zaidi kuliko walivyoingia magerezani. Mchakato huu unakwenda sanjari na uboreshaji wa huduma kwa wafungwa magerezani. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya tafakari ya kina, ili hatimaye, kufuta kabisa adhabu ya kifo, ili kudumisha haki msingi za binadamu.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna nchi 105 ambazo zimekwishafuta adhabu ya kifo na nyingine 43 kwa miaka mingi hazijawahi kutekeleza adhabu ya kifo, ingawa imeandikwa kwenye Katiba na Sheria za nchi husika. Hata hivyo adhabu ya kifo katika kipindi cha miaka miwili imetekelezwa katika nchi 22 duniani. Nchi nyingi kwa sasa zinaendelea kuangalia uwezekano wa kufuta adhabu ya kifo, changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.