2016-04-11 11:08:00

Halmashauri nchini Tanzania kutumia 10% ya Pato lake kuwekeza kwa vijana!


Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amesema Mkurungezi yeyote wa Halmashauri nchini atakayeshindwa kutenga asilimia 10% ya mapato kwa ajili ya wanawake na vijana ataondolewa. Amesema suala la kila Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na vijana kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi ni la lazima na si hiari.

Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema hayo Jumapili tarehe 10 Aprili, 2016 alipokuwa anazungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Kitandi, Mtimbo, Likunja, Nkowe na Namahema ambako alifanya mikutano ya hadhara. “Halmashauri ambayo itashindwa kutenga asilimia 10 kwa maana asilimia tano kwa ajili ya vijana na tano kwa ajili ya akinamama Mkurugenzi wake atakuwa anatafuta safari,” amesema Waziri Mkuu, Majaliwa.

Waziri Mkuu, Majaliwa yupo wilayani Ruangwa, Lindi kwa ajili ya ziara ya kikazi inayolenga kukagua shughuli za maendeleo, ambapo amewasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kutimiza wajibu wao na serikali haitamvumilia yeyote atakayeshindwa. Pia Waziri Mkuu, Majaliwa amewataka wananchi hao kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili zitakapofika sh milioni 50 za kila kijiji zilizoahidiwa na Rais, Dk. John Magufuli waweze kunufaika.

Amesema fedha hizo ambazo zitatolewa kuanzia mwezi Julai mwaka huu zitagawiwa katika vikundi mbalimbali vilivyosajiliwa na si kwa mtu mmoja mmoja hivyo amewataka watendaji wa kata na vijiji kuwahamasisha wananchi kujiunga katika vikundi. Katika hatua nyingine Waziri Mkuu, Majaliwa amesema serikali imefuta tozo tano kati ya tisa za zao la korosho zilizokuwa kero ya muda mrefu na kufanya wakulima wachukie mfumo wa Stakabadhi ghalani.

Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu. 








All the contents on this site are copyrighted ©.