2016-04-24 09:08:00

Upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma ni utambulisho wa Mkristo!


Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi! Upendo ni utambulisho na ushuhuda wa wafuasi wa Kristo unaopaswa kupyaishwa kila wakati kwa kujikita katika ushuhuda, urafiki na uaminifu kwa Kristo Yesu. Huu ni upendo unaomwilishwa katika matendo kwa wakristo kuendelea kuwa ni wanafunzi wa shule ya maisha, daima wakijifunza kupenda kwani hili ni jambo jema linalowawezesha watu kuwa na furaha.

Lakini, upendo una gharama na machungu yake; ni zawadi na sadaka inayoshuhudiwa na wazazi, walezi na walimu, ili kuwawezesha watoto wao kuwa na furaha ya maisha. Kupenda maana yake ni kujisadaka maisha, muda, urafiki, karama na mapaji mbali mbali ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mja wake! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumapili, tarehe 24 Aprili 2016 wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa watoto ambao kwa sasa wako mjini Roma.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwafafanulia watoto hawa kwamba, Kristo ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na ukarimu, changamoto kwa watoto hawa kumshukuru kila siku ya maisha bila kuchoka wala kusahau, kwani hata wakisahau kushukuru wakumbuke kwamba, amewajalia zawadi kubwa ya maisha ambayo ni uaminifu endelevu katika urafiki, ambao kamwe hautaondoshwa kwao, hata kama watoto hawa watakengeuka na kumsamahau Kristo, ataendelea kuwa karibu yao na kuwapenda, ili waweze kukua na kukomaa vyema.

Kristo anawathamini na kuwajali na anataka kuwa pamoja nao, kama alivyofanya kwa wafuasi wake! Anawaangalia machoni, anawaita kwa majina na kuwataka kumfuasa, tayari kushusha nyavu zao kwa kuwa na imani na Neno la Yesu. Hii ni changamoto kwa watoto kutumia vyema karama na vipaji ambavyo wamekirimiwa katika maisha, ili kuvitumia pamoja na Kristo pasi na woga na kwamba, Yesu anaendelea kuwa na uvumilivu, akisubiri jibu lao la “Ndiyo”!

Baba Mtakatifu anawakumbusha watoto hawa kwamba, katika umri wao kuna tamaa ya kupenda na kupendwa! Wakithubutu kwenda kwenye shule ya Yesu atawafundisha namna bora ya kupenda na kupendwa, kwa kuwapatia nia njema ya kupenda bila kummiliki mtu; kumpenda mtu bila ya kumgeuza kuwa ni mali yako binafsi, bali kwa kumwachia uhuru pamoja na kuachana na tabia ya kupenda kile unachotaka kupenda, matokeo yake ni utupu na kudumaa katika maisha, mambo ambayo yanajitokeza kwa kiasi kikubwa katika ulimwengu mamboleo. Watoto hawa wakithubutu kuisikiliza sauti ya Kristo kwa umakini mkubwa, atawafunulia siri ya wema kwa kuwahudumia wengine, maana yake: kuwaheshimu, kuwalinda na kuwasubiri!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, katika umri wao, watoto hawa wana kiu kubwa ya uhuru, lakini wanapaswa kufahamu maana ya uhuru, bila kujifunga katika ubinafsi; kujitenga na wengine; kwa kuwa na urafiki unaojikita katika ukweli na uwazi. Uhuru ni zawadi inayomwezesha mtu kuchagua kilicho chema, kwa kutekeleza mapenzi ya Mungu hata kama kunahitajika sadaka. Maamuzi thabiti ndiyo yanayosaidia kutekeleza ndoto kubwa za watu katika maisha.

Wasikubali wajanja wachache kuwapokonya utajiri wa maisha yao ya ujana; watu wanaotaka kuwakejeli kwa kuwaonesha kuwa wao ni “mastar” wa sinema au wanapovaa mavazi ya mitindo ya kisasa, lakini watambue kwamba, maisha yao yana thamani kubwa kuliko hata simu ya mkononi ambayo haiwezi kuwasaidia kuwa huru na wakomavu katika upendo, kwani upendo ni zawadi inayojikita katika uhuru kamili; inawajibisha na inadumu katika maisha.

Hii ni dhamana inayopaswa kufanyiwa kazi kila siku ya maisha kwa mtu anayetambua kuota ndoto kubwa, kijana asiyethubutu kuota ndoto, huyo atambue kwamba, tayari ameanza kula pensheni ya maisha ya uzeeni. Upendo unarutubishwa kwa njia ya imani, heshima na msamaha; mambo yanayomwilishwa katika uhalisia na maamuzi ya maisha. Baba Mtakatifu anawakumbusha watoto hawa kwamba, Yesu Kristo ana ufunguo wa siri ya ufanisi na ukuaji wa kweli katika maisha: kwa kushiriki Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, kwani kwa njia ya Sakramenti hizi, Yesu anawakirimia chakula cha uzima wa milele, msamaha na amani ya ndani, mwaliko kwa kumwilisha upendo huu katika uhalisia wa maisha.

Watoto watazame na kulitafakari Fumbo la Msalaba na kushikamana na Yesu, ili aweze kuwainua pale watakapojikwaa na kuanguka kwani hii ni sehemu ya udhaifu na mapungufu ya binadamu. Yesu anataka kuwaona wakiwa wamesimama imara! Kuanguka wataanguka, lakini jambo la msingi si kuendelea kukaa pale walipoangukia, bali kusimama na kusonga mbele kwa msaada wa marafiki, wazazi, walezi, ndugu na jamaa. Baba Mtakatifu anatambua kwamba, watoto hawa wana uwezo wa kujenga urafiki na wema, kwa kuendelea kushirikiana na wengine katika mchakato wa ujenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi! Kamwe, wasigombane na wengine, bali watambue kwamba, wana utajiri mkubwa katika maisha ya ujana wao wasiwe na hofu ya kuchakarika katika maisha, bali waendelee kufanya mazoezi katika hali ya unyenyekevu kama wafanyavyo wanamichezo wanaotaka kufikia malengo makubwa ya maisha. Matendo ya huruma yawe ni mazoezi yao kila siku, ili waweze hatimaye, siku moja kuwa ni washindi wa maisha na upendo na kwa njia hii wataweza kutambulikana kuwa ni wafuasi wa Kristo Yesu na furaha yao itakuwa timilifu zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.