2016-06-06 08:37:00

Mbinu mkakati wa kupambana na uhalifu dhidi ya ubinadamu!


Jopo la Majaji na Mahakimu waliokuwa wanashiriki katika mkutano wa kimataifa ulioandaliwa na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii, ili kuibua mbinu mkakati wa kupambana na biashara haramu ya binadamu pamoja na uhalifu wa magenge limehitimisha mkutano huu kwa kutoa tamko rasmi. Jopo hili linatambua mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko, viongozi wakuu wa dini pamoja na Mameya wa miji mikuu mintarafu biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Haya ni matukio yanayofumbwatwa kwenye kazi za suluba, ukahaba na pamoja na biashara haramu ya viungo vya binadamu, mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu. Mapambano dhidi ya changamoto hizi ni dhamana ya kimaadili kimataifa kama ilivyopitishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika tamko lao mintarafu Maendeleo Endelevu. Haki dhidi ya uhalifu inafumbata pia haki jamii pamoja na haki mazingira kama inavyofafanuliwa kwa kina na mapana na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si.

Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini; kuwasaidia na kuwarejesha tena katika maisha ya kijamii waathirika wa utumwa mamboleo na biashara haramu ya binadamu. Lengo ni kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, pamoja na kuwajengea nguvu ya kiuchumi, ili wasirejeshwe tena katika mzunguko wa utumwa mamboleo au mambo yanayowadhalilisha kama binadamu, ili hatimaye, kuchangia kikamilifu katika ustawi wa maendeleo yao na jamii wanamoishi!

Jopo na Majaji na Mahakimu katika mkutano huu ambao pia ulimshirikisha Baba Mtakatifu Francisko wameibua mambo makuu kumi, yanayopaswa kutekelezwa ili kupambana kikamilifu na biashara haramu ya binadamu pamoja na uhalifu wa magenge. Jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ushirikiano wa kutosha kati ya Mfumo wa Kimahakama na Jeshi la Polisi ili kusaidia mchakato wa kupambana na uhalifu, kuimarisha taasisi za kimataifa katika mapambano dhidi ya wafanyabiashara ya binadamu sanjari na kulinda haki msingi za binadamu.

Baada ya Jumuiya ya Kimataifa kutambua athari za utumwa mamboleo mintarafu Itifaki ya Palermo dhidi ya biashara haramu ya binadamu, kazi za suluba na ukahaba kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, inapaswa kutekelezwa kwa vitendo. Mali iliyotaifishwa kutoka kwa wale wanaojihusisha na vitendo hivi isaidie kutoa huduma kwa waathirika wa vitendo hivi vya kinyama. Wahusika wa vitendo vya utakatishaji wa fedha haramu, washughulikiwe kisheria sanjari na kuwadhibiti wala rushwa na mafisadi.

Kuna haja ya kutoa ushirikiano wa dhati kwa waathirika wa vitendo hivi vya kinyama, ikiwa ni pamoja na msaada wa kisheria; ulinzi na usalama; msaada wa huduma ya afya pamoja na huduma za kijamii, hasa kwa waathirika wasiokuwa na nyaraka maalum. Waathirika wahamasishwe kushirikiana vyema na vyombo vya ulinzi na usalama kama mashuhuda, kwa kuwahakikishia usalama pamoja na kuwapatia msaada wa kiufundi kwa kutumia programu za ulinzi kimataifa.

Kwa waathirika ambao hawana vibali vya kuishi, wasaidiwe kupata vibali ya muda; wapewe msaada wa kisheria pamoja na kupata huduma za kimahakama ili kutetea na kulinda haki zao msingi. Pale inapowezekana wasaidiwe kupata mafunzo ya kazi ili waweze tena kurejea katika mzunguko wa nguvu kazi. Mchakato wa kuwatambua na kuwasaidia waathirika wa utumwa mamboleo uharakishwe zaidi.

Biashara haramu ya viungo vya binadamu inapaswa kutambuliwa kuwa ni uhalifu na hivyo kushughulikiwa kitaifa na kimataifa; pamoja na kuibua mbinu mkakati wa kudhibiti biashara hii haramu. Wateja wa utalii wa ngono hawana budi pia kushughulikiwa kisheria na kuwa ni sehemu ya mbinu mkakati wa kupambana na biashara haramu ya binadamu kama inavyopaswa pia kwa waajili wanaowafanyisha watu kazi za suluba. Wafanyabiashara haramu ya binadamu watambuliwe na kushugulikiwa kisheria. Mahakama iwe makini kuwashughulikia wageni wasiokuwa na vibali vya kuishi, ili wasitumbukizwe tena katika vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.