2016-08-02 15:48:00

Kilele cha Jubilei ya miaka 800 ya Msamaha wa Assisi


Wafranciskani sehemu mbali mbali za dunia wanaadhimisha Jubilei ya miaka 800 ya Msamaha wa Assisi, tukio ambalo litapambwa kwa namna ya pekee na uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko atakapotembelea Assisi hapo tarehe 4 Agosti 2016 ili kusali na kutafakari kwenye Kikanisa cha “Porziuncola”. Wakuu wa Mashirika ya Kifranciskani katika maadhimisho haya wanawataka wanashirika wote pamoja na watu wenye mapenzi mema kuwa na aibu takatifu kutokana na ukweli kwamba, jitihada za kutaka kukuza na kudumisha amani, usalama na ustawi kati ya watu zinaendelea kugonga mwamba.

Wafranciskani wamwombe Mwenyezi Mungu neema na baraka ya kuwa na kipaji cha ugunduzi, ili kuweza kuimba utenzi utakaoeleweka na watu wa kizazi hiki katika jitihada za kutaka kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho. Wakuu wa Mashirika ya Kifranciskani katika ujumbe wao kwa ajili ya maadhimisho haya wanasema, tarehe 2 Agosti 2016 ni siku maalum ya kujipatia rehema kwa wale wote watakaokuwa wametimiza masharti yanayotolewa na Mama Kanisa.

Pili, Jubilei hii inakwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iliyotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko aliyemchagua Mtakatifu Francisko wa Assisi kuwa ni msimamizi wake katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Maadhimisho haya iwe ni fursa ya kutafakari kwa kina na mapana dhana ya huruma ya Mungu na msamaha mintarafu tasaufi ya maisha ya Wafranciskani.

Wakuu wa Mashirika ya Kifranciskani wanakaza kusema, huruma ni neno muhimu sana katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko, changamoto kwa waamini kukimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, lakini pia kuwa na huruma kwa jirani zao kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma. Huruma na msamaha ni  chanda na pete kwani ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana katika maisha ya kiroho. Kimsingi, huu ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu yanayojikita katika upendo kwa Mungu na jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.