2017-01-03 11:22:00

Waziri wa mazingira nchini Burundi auwawa kikatili!


Burundi imeuanza Mwaka 2017 kwa mauaji ya Emmanuel Niyonkuru, mwenye umri wa miaka 54 ambaye pia alikuwa ni waziri wa Mazingira nchini Burundi. Jeshi la Polisi nchini humo linasema, Waziri Niyonkuru aliuwawa kwa kupigwa risasi wakati alipokuwa anarejea nyumbani kwake katika kitongoji cha Rohero. Hadi sasa taarifa za Jeshi la Polisi zinasema kwamba, kuna mwanamke mmoja anayeshikiliwa na Polisi kwa tuhumza za kuhusika na mauaji ya Waziri Niyonkuru.

Wachunguzi wa mambo wanasema, haya ni mauaji ya kwanza kufanywa kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa Serikali ya Burundi, tangu machafuko ya kisiasa yalipojitokeza nchini humo kunako mwaka 2015, Rais Pierre Nkurunziza alipoamua kuwania kiti cha Urais na hatimaye, kuchagua tena kwa awamu ya tatu mfululizo kinyume cha Katiba na Makubaliano ya Arusha, Tanzania yaliyositisha vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi. Kwa kuhofia kwamba, Rais Nkurunziza angeweza kufikishwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, Burundi kunako mwaka 2016 ikajitoa kutoka kwenye Mahakama hii.

Wimbi la machafuko haya yanayoanza kuwagusa na kuwatikisa viongozi wakuu Serikalini ni kutokana na tamko lililotolewa hivi karibuni na Rais Pierre Nkurunziza anayefikiria bado kuwania tena uongozi kwa awamu ya nne, muda utakapofika! Wachunguzi wa masuala ya kisiasa nchini Burundi wanasema, tamko hili limewatia watu “kichefu chefu”. Takwimu zinaonesha kwamba, tangu mwaka 2015 kulipoteka machafuko ya kisiasa nchini Burundi, zaidi ya watu 500 wameuwawa na wengine zaidi ya 300, 000 wamelazimika kuikimbia nchi yao ili kutafuta usalama wa maisha kwenye nchi jirani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.