2017-05-10 15:33:00

Wanasiasa msijitafutie umaarufu kwa matatizo ya wakimbizi na wahamiaji


Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji inaweza kuvaliwa njuga kwa kujikita katika ukarimu na udugu mambo msingi yanayofumbatwa katika Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa kuheshimu na kuthamini tamaduni, mila na mapokeo ya wakimbizi na wahamiaji, tayari kujikita katika mchakato utakaosaidia kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Wakimbizi na wahamiaji wana mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na uzalishaji wa rasilimali watu, muhimu sana kama chanzo cha nguvu kazi katika huduma na uzalishaji. Licha ya mchango mkubwa unaotolewa na wakimbizi pamoja na wahamiaji, lakini bado wanabaguliwa sana katika nchi zinazowapatia hifadhi! Hapa inapaswa kukumbukwa kwamba, hawa ni watu wenye utu na heshima yao na ni sawa na binadamu wengine wote! Wanajikuta katika mazingira hatarishi kutokana na sababu mbali mbali!

Huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss wakati wa kuchangia mada kuhusu: usalama, wahamiaji; mifumo mbali mbali ya ubaguzi, ikiwemo: ubaguzi wa rangi, ukosefu wa maridhiano na woga usiokuwa na mashiko wala mvuto! Haya ni mambo yanayomwangalia binadamu kwa “jicho la kengeza” kwa kusukumwa zaidi na masilahi ya kiuchumi, kinyume kabisa cha utu, heshima na usawa wa binadamu wote.

Hapa kuna haja ya kuwa na takwimu sahihi kuhusu wakimbizi na wahamiaji ili kupata hali halisi ya wakimbizi na wahamiaji na sababu msingi zinazoendelea kuchangia uwepo wa wimbi hili kubwa katika karne ya ishirini na moja. Askofu mkuu Ivan Jurkovic anaonya kwamba, umaarufu wa baadhi ya wanasiasa wa kutaka kujijenga kisiasa kwa kutumia migongo ya wakimbizi na wahamiaji inaficha ukweli wa sababu msingi zinazowafanya watu wengi kuamua kufanya maamuzi machungu katika maisha kwa kuzikimbia na kuzihama nchi zao!

Umaskini wa hali na kipato; baa la njaa na magonjwa; ukosefu wa fursa za ajira; vita, kinzani, mipasuko na dhuluma za kidini ni kati ya mambo yanayoendelea kuchangia uwepo wa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu alivionya vyombo vya habari kuhakikisha kwamba, vinatoa habari kuhusu ukweli wa shida na mahangaiko ya wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotaka hifadhi ya kisiasa. Mambo haya kamwe yasichanganywe. Itifaki, mikataba na makubaliano yaliyofikiwa kwenye Jumuiya ya Kimataifa yanapaswa kutekelezwa kwa umakini mkubwa ili kusaidia mchakato wa kuondokana wimbi kubwa la mifumo ya kibaguzi inayotaka kupaka matope mustakabali wa wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.