2017-10-19 15:10:00

Jubilei ya Miaka 50 ni kipindi cha: Umoja, Utakatifu na Upatanisho


Kadiri ya Mapokeo ya tangu Agano la Kale, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 kilikuwa ni kipindi muafaka cha kuwaachia watu huru na kwa upande wa Makanisa ni wakati wa kuondokana na tabia ya kudhaniana vibaya. Baraza la Wamethodist Duniani linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya majadiliano ya kiekumene na Kanisa Katoliki na matunda yake ni: uvumilivu na majadiliano ya kidugu yanayowafanya waamini wote kujisikia kwamba, wako nyumbani na wala hakuna mgeni ndani ya Kanisa, kwani wote ni wafuasi wa Kristo, dhamana waliyojitwalia kwa kupokea Sakramenti ya Ubatizo. Kwa njia ya neema ya Ubatizo, wote wanakuwa ni watu wa nyumbani kwa Mungu!

Haya yasemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 19 Oktoba 2017 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Wamethodisti Duniani kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 50 ya majadiliano ya kiekumene na Kanisa Katoliki, changamoto kubwa iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican waliokazia umuhimu wa kuandamana kwa pamoja kwa kuutamani ukweli, kwa upendo na unyenyekevu. Majadiliano ya kweli yanawapatia waamini fursa ya kukutana na jirani zao katika unyenyekevu na ukweli; ili kujifunza pia kutoka kwa wengine kwa moyo wa uaminifu na unyofu.

Baba Mtakatifu anatambua kwamba, wao ni ndugu katika Kristo Yesu, ambao wametengana lakini wanaweza kujifunza na kuanza kusonga mbele kwa kutembea kwa pamoja, huku wakitambua kwamba, safari yao inapata baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni chemchemi na hatima ya kila baraka zote. Huu ni muda wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha kama alivyofanya John Wesley aliyewasaidia jirani zake kukumbatia utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wake.

Aliwahimiza watu kusoma Bibilia Takatifu na Kusali sana, ili kumfahamu Kristo Yesu, changamoto hata kwa Wakristo wa nyakati hizi kufurahia ushuhuda unaobubujika kutoka katika utakatifu wa maisha. Inafurahisha kuona umati mkubwa wa Wakristo ukizaa matunda mengi zaidi kwa njia ya ushuhuda wa Injili ya Kristo, changamoto kwa sasa ni kuimarishana wao kwa wao kama kielelezo cha ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika upendo wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anasema, Jubilei ni kipindi cha kujenga na kudumisha umoja na Mwenyezi Mungu; kutafuta na kuambata utakatifu wa maisha kwa kujenga umoja, udugu na upendo kwa jirani, tayari kufungua ukurasa mpya unaojikita katika upatanisho na umoja kamili chini ya Kristo mchungaji mkuu. Upatanisho iwe ni zawadi kwa Makanisa na ulimwengu katika ujumla wake, kwa kuhakikisha kwamba, wakristo wanakuwa  kweli ni vyombo vya upatanisho, muujiza unaotendwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Ni Roho Mtakatifu ndiye anayeratibu karama na kuzielekeza katika umoja pasi na ulazima wa kufanana. Wakristo wanapaswa kushikamana kama wakati ule, Mitume walipokuwa wanamngoja Roho Mtakatifu, ili wote kama ndugu, waweze kushirikishana safari hii!

Baba Mtakatifu Francisko amechukua fursa hii kuishukuru Tume ya Majadiliano kwa kazi kubwa inayofanya kwa kutiwa shime na Baraza la Wamethodisti Duniani ili kuendeleza mchakato wa majadiliano na kwamba, katika kipindi cha miaka 50 waamini wa Makanisa haya mawili wamebahatika kufahamiana kwa ukaribu zaidi. Dhamana kubwa kwa sasa iliyoko mbele yao ni kuhakikisha kwamba, wanashikamana kama ndugu katika Kristo, huku wakionesha unyenyekevu katika matumaini na hatimaye, kuibua mbinu mkakati utakaowawezesha kutambua mintarafu neema ya Mungu, kwa kushiriki tena kuumega Mkate wa uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.